![]() |
| Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha: Mwananchi |
Dar es Salaam: Mwanasheria wa kujitegemea
nchini, Fatma Karume amemshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein
kuachia madaraka. “Dk Shein lazima aondoke kwa sababu kuendelea kubaki
madarakani ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi,” alisema
Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Fatma
alisema kuwa mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo
yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria kufanya
hivyo.
Fatma alisema Jecha hana mamlaka kikatiba
na kisheria kufuta matokeo hayo kwa kuwa maamuzi kama hayo yanatakiwa
kufanywa na ZEC yenye mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watano;
watatu kutoka CCM na wengine wawili kutoka CUF.
“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na
wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika, akidi ilitimia na jambo hilo
likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe
wengine. Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa
sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila kupata akidi hiyo,”
alifafanua Fatma.
Mwanasheria huyo alisema kuwa amekuwa
akiwasikia baadhi ya wana CCM Zanzibar wakisema kuwa Jecha ndiyo tume na
tume ndiyo Jecha, hivyo ana haki ya kufuta uchaguzi.
Lakini Fatma alisema Jecha hana mamlaka
kusema jambo ambalo halijakubaliwa na tume. Alipoulizwa ikiwa hatua ya
aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Seif Sharrif Hamad ya kutangaza
matokeo aliyodai yalimpa ushindi si kosa, Fatma alisema, “Sikumuona
Maalim Seif alipokuwa anatangaza matokeo hayo hivyo sijui kama
alijitangaza kuwa mshindi au alitangaza matokeo kama yalivyobandikwa
kwenye vituo.
“Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia
mgombea anaweza kuona mwelekeo wa matokeo na akampigia mwenzake
kumpongeza. Nadhani Maalim Seif alisoma jumla ya matokeo ya uchaguzi
kama yalivyobandikwa kwenye vituo, hivyo hilo si kosa ati,” alisema na
kuongeza:
“Ninasikitishwa na tabia hii. Sikutegemea
kama CCM watatumia nguvu kutaka kubaki madarakani kwa njia hii.
Sikutegemea kama watavuruga katiba…ndiyo maana nina huzuni.”
Jambo jingine alilosema litazua mgogoro
Zanzibar ni mamlaka yenye haki ya kuidhinisha fedha za uchaguzi wa
marudio ikiwa watalazimisha ufanyike. “Kisheria fedha hizo ni lazima
zikubaliwe na Baraza la Wawakilishi.
Baraza lipo wapi? Ili mtu awe waziri
lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Rais alivunja Baraza Agosti
na kwa hiyo hadi ilipofika siku ya kuapishwa rais mpya, Zanzibar hakuna
Baraza wala Waziri. Ina maana fedha za wananchi zinatumiwa bila idhini
ya Baraza, ” alisema.
Alisema kinachofanyika Zanzibar ni
‘ukoloni’ wa watu weusi dhidi ya watu weusi ambao unawakosesha
Wazanzibari haki yao msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka. “Hali si
shwari Zanzibar.
Watu wamekata tamaa kwa sababu unapokuwa
na Serikali ambayo inanyang’anya haki ya wananchi ya kupiga kura,
kuandamana, watu wanakosa imani na Serikali hiyo,” alisema.
Kurudia uchaguzi Kuhusu kurudiwa uchaguzi
nchi nzima, Fatma alisema ulipofanyika uchaguzi mwaka 2000 ambao Amani
Karume aligombea kwa mara ya kwanza, zilitokea dosari katika majimbo 10
ya Unguja.
CUF walipotaka uchaguzi urudiwe nchi nzima, CCM chini ya Benjamin Mkapa waligoma wakasema ni katika majimbo yenye dosari tu.
“Nini kimetokea mwaka huu? Kama dosari
zilijitokeza Pemba kama wanavyodai kwa nini urudiwe Unguja? Kwa nini
hawataki kutumia uamuzi wa mwaka 2000 wa kurudia maeneo yenye dosari
tu?” alihoji.
“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha
Hard Talk cha BBC akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian uchaguzi hauwezi
kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo. Kwa nini leo mambo
yamebadilika na CCM inataka uchaguzi mpya?” alihoji.
Fatma ambaye alikataa kueleza msimamo
wake kisiasa, alisema iwapo uchaguzi huru na wa haki utafanyika leo
Zanzibar, CCM haiwezi kushinda kwa sababu Wazanzibari wanajionea yale
ambayo wanafanyiwa na chama hicho.
“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu
ilishindwa kuwashawishi watu wake na badala inawakemea, ikawanyima haki
zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini
ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” alisema.
Sherehe za Mapinduzi Wakati zikiwa
zimesalia siku nne kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Sikukuu
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma alisema kwa hali ilivyo haina maana
kutokana na CCM kung’ang’ania kukaa madarakani kwa nguvu.
“Ninajisikia kusalitiwa. Madhumuni ya
Mapinduzi haikuwa kuiweka CCM madarakani milele bali kurejesha madaraka
kwa wananchi,” alisema.
Alisema aliambiwa kuwa waliofanya
mapinduzi (wakiongozwa na Abeid Amani Karume) walitabiri kuwa ipo siku
Zanzibar itakuwa na uchaguzi au Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini CCM
hawataki.
“Wakati hao waliofanya mapinduzi wakisema
hivyo, CCM haikuwepo, ilikuwepo ASP. Hao ASP hawakuwa wakijiaminisha
kuwa watakaa madarakani milele,” alisema.
“Wakati tunaadhimisha mapinduzi ya
Zanzibar, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa malengo ya mapinduzi hayo
yalikuwa ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuweka misingi ya
kidemokrasia lakini CCM wamevuruga,” alisema Fatma.
Chanzo: Mwananchi

Post a Comment Blogger Facebook