Unknown Unknown Author
Title: MAGUFULI AMSHAWISHI MO KUJENGA KIWANDA SINGIDA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
 Dk John Magufuli akihutubia wananchi wa Mjini Mtwara. MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli amemshawishi aliyekuwa ...
 Dk John Magufuli akihutubia wananchi wa Mjini Mtwara.
MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli amemshawishi aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Mjini, Mohammed Dewji, kujenga kiwanda mkoani humo, ili pamoja na mambo mengine, kupunguza uhaba wa ajira.
Amedai Dewji maarufu kwa jina la MO ambaye kwa sasa ni bilionea mfanyabiashara wa mwaka wa Afrika, katika kipindi chake cha ubunge miaka 10 iliyopita ameonesha mapenzi makubwa na ya aina yake kwa wakazi wa jimbo la Singida na mkoa kwa ujumla.
Alisema kutokana na ukweli huo, sasa anapaswa kuhamishia mapenzi hayo kwa kujenga kiwanda mkoani Singida kitakachoajiri vijana, na pia kuinua pato la mkoa na taifa kwa ujumla. Mgombea urais huyo aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Peoples mjini Singida na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa jimbo la Singida na maeneo ya jirani.
“Katika kipindi chako cha ubunge umeonesha uzalendo wa hali ya juu, umewatumikia vema wananchi wa jimbo la Singida mjini. Ndio maana hadi sasa bado wana mapenzi makubwa sana kwako, naomba uwajengee kiwanda.
Nakuhakikishia mimi binafsi napenda wawekezaji wazalendo wanaoipenda nchi yao na wewe ni mmoja wao,” alisema Dk Magufuli. Aidha, Dk Magufuli ameahidi kumpa ushirikiano pindi atakapohitaji kuwekeza katika viwanda mkoani Singida.
Akisisitiza, alisema, “Dewji nakuomba sasa ikiwezekana jenga hata viwanda vitatu ili wananchi wa mkoa wa Singida wapate ajira. Nitakuunga mkono kwa asilimia 100. Kama ni kibali unataka, nitakupa leo hii kwa kuwa mmenihakikishia nitakuwa rais wa tano”.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni, Dewji aliwaahidi wakazi wa jimbo la Singida Mjini kwamba ataendelea kushirikiana nao katika kulipaisha jimbo hilo kimaendeleo. “Mimi nimezaliwa hapa nyumbani kwetu Singida Mjini na kitovu changu kimezikwa hapa hapa.
Kutoka chini ya sakafu ya moyo wangu, niwahakikishie kwamba nalipenda sana jimbo letu hili la Singida Mjini. Nitaendelea kulisaidia kwa hali na mali kadri uwezo utakavyoniruhusu”, alisema na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.
Dewji alisema nia yake ya kuomba ubunge huko nyuma, lengo ilikuwa na kutaka kushirikiana na wananchi kuliletea maendeleo jimbo la Singida Mjini, na sio kujinufaisha binafsi. ”Jimbo sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote muhimu.
Najua bado tuna mengi ya kufanya ya kimaendeleo kwa kizazi cha sasa na kile kijacho. Kwa hiyo sitowaacha, tutaendelea kushirikiana kuliendeleza jimbo la Singida mjini ili liwe mfano wa kuigwa na majimbo mengine katika masuala ya kimaendeleo”, alisema.
Baadhi ya wakazi wa jimbo la Singida Mjini wamedai Dewji ataendelea kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo, kutokana na tabia yake ya kuwapenda wananchi wote na hakuwa na chembe chembe ya ubaguzi.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

 
Top