Wagombea urais wawili wakuu wa urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump wanakaribiana sana katika matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.
Clinton ameshinda Virginia naye Trump akashinda Ohio, Florida, na North Carolina.
Kwa sasa Trump ana kura 222 za wajumbe na Clinton 209. Mshindi anahitaji kura 270 za wajumbe.
Lakini
mgombea wa Republican Bw Trump ameshinda majimbo mengi ya kusini mwa
Marekani naye Bi Clinton akashinda majimbo ya kaskazini mashariki mwa
nchi hiyo, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la ABC News.
Chama cha Republican kinaonekana kuwa njiani kuhifadhi wingi wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.
![]() |
Donald Trump alipakia picha hii kwenye Twitter, yake, mgombea mwenza wake na jamaa na marafiki wakifuatilia matokeo New York. |
Kama ilivyotarajiwa, Bw Trump ameshinda katika ngome za Republican
katika majimbo ya Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana,
West Virginia, Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas, ABC News
wanakadiria.
Bw Trump pia anakadiriwa kushinda Arkansas, Kansas, North Dakota, South Dakota, Montana na Wyoming.
Shirika
hilo linakadiria Bi Clinton atashinda ngome za Democratic majimbo ya
New York, New Jersey, Connecticut, Massachusetts, Maryland, Vermont,
Delaware, Illinois, Rhode Island na District of Columbia.
Mshindi anahitaji kupata kura 270 kati ya jumla ya kura 538 za wajumbe ndipo atangazwe mshindi.
Upigaji kura umemalizika katika majimbo 39 na matokeo kamili
yalitarajiwa mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT Jumatano - Saa moja
asubuhi Afrika Mashariki), upigaji kura utakaomalizika Pwani ya
Magharibi.
Matukio mengine makuu:
- Bodi ya Uchaguzi Carolina Kaskazini imekubali kuongeza muda wa kupiga kura maeneo manane wilaya ya Durham ambapo kuna milolongo mirefu ya wapiga kura.
- Mgombea wa Republican aliyeshindwa kwenye mchujo Marco Rubio amehifadhi kiti chake cha useneta Florida
- Thamani ya pesa za Mexico, peso, imeshuka sana baada ya Trump kuonekana akiongoza Florida
- Mtu mmoja alifariki kwenye ufyatulianaji wa risasi karibu na kituo cha kupigia kura jimbo la Azusa, California. Watu watatu walijeruhiwa.
Bw Trump, tajiri kutoka Manhattan, na Bi Clinton, anayetaka
kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani, walipiga kura mapema Jumanne
katika jiji la New York.
Bw Trump alizomewa alipofika kupiga kura yake Manhattan, akiandamana na mkewe, Melania, na bintiye, Ivanka.
Wawili hao wamekuwa wakifuatilia matokeo kutoka jiji la New York.
![]() |
Clinton amepakia picha hii, pamoja na ujumbe wa shukrani kwa watu wote, licha ya matokeo ya usiku wa leo
|
Bi Clinton atahutubia wafuasi Javits Centre, Manhattan naye Bw Trump atahutubu katika hoteli ya Hilton Midtown.
Maafisa wa polisi zaidi ya 5,000 wametumwa jijini New York kuimarisha usalama.
Utafiti
wa maoni wa baada ya upigaji kura, uliofanywa na ABC News, unaonyesha
wapiga kura 61% hawampendi Bw Trump nao 54% ndio hawampendi Bi Clinton.
Mapema Jumanne, Bw Trump kwa mara nyingine alikataa kusema iwapo atakubali matokeo.
"Tutaangalia tuone vile mambo yatakuwa," aliambia Fox News, huku akidai kwamba kumekuwa na kasoro hapa na pale kwenye uchaguzi.
"Ninataka kila kitu kiwe wazi."
Katika
baadhi ya vituo, mitambo ya kupigia kura ilifeli na kwingine kukawa na
milolongo mirefu, lakini yalionekana kuwa matatizo ya kawaida.
Bw
Trump, aliyezua utata kuhusu kuaminika kwa shughuli ya uchaguzi kwa
kudai kura "zitaibwa" mapema, pia amewasilisha kesi ya dharura Nevada.
Maafisa
wa Republican wamemshtaki msajili wa wapiga kura wilaya ya Clark,
wakidai jimbo hilo lilifungua vituo vya kupigia kura muda mrefu kuliko
inavyofaa.
Lakini jaji ameitupilia mbali kesi hiyo.
Kando na kura za urais, Wamarekani wamekuwa pia wakipiga kura za Maseneta, wabunge wa Bunge la Wawakilishi na Magavana.
Viti
vyote 435 Bunge la Wawakilishi vilikuwa vinashindaniwa, na ABC News
wanakadiria kwamba bunge hilo litabaki chini ya udhibiti wa Republican.
Lakini
theluthi moja ya viti Seneti, ambao Republican wamekuwa wanaongoza, pia
vinashindaniwa, na Democratic wanatumai wanaweza kudhibiti bunge hilo.
Jumla ya Wamarekani 45 milioni, idadi kubwa zaidi kuliko awali, walijitokeza kupiga kura mapema.
Bw Trump na Bi Clinton wanapigania kumrithi Barack Obama wa Democratic.
Rais Obama haruhusiwi kuwania kikatiba baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka minne.
Rais mpya ataapishwa tarehe 20 Januari 2017.




Post a Comment Blogger Facebook