Marekani imelaani kukamatwa na kuzuiwa kwa muda kiongozi wa upinzani,
Kizza Besigye, anayetumai kuifikisha kikomo miaka 30 ya utawala wa rais
wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni.
Huku kura zikiendelea kuhesabiwa nchini Uganda kufuatia uchaguzi wa rais
na bunge uliofanyika hapo jana, Marekani imeilaani vikali serikali ya
Uganda baada ya maafisa wa usalama kumkamata kwa muda mfupi mgombea
urais wa upinzani Kizza Besigye. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya
Marekani John Kirby alisema kitendo hicho kinatilia shaka uwajibikaji wa
Uganda kufanya uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi.
Besigye ambaye ni mgombea wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa miongoni
mwa wagombea saba wanaoshindana na Rais Museveni, alitiwa mbaroni wakati
alipokuwa akichunguza madai ya wizi wa kura uliofanywa na chama tawala
cha National Resistance Movement, NRM.
Msemaji wa chama cha Besigye, Forum for Democratic Change, FDC, Semuju
Nganda, alisema kiongozi huyo alikamatwa wakati alipokuwa akifanya
uchuguzi katika kituo kisicho halali kilichokuwa kikisimamiwa na maafisa
wa usalama katika mji mkuu, Kampala.
Msemaji wa polisi Fred Enaga alithibitisha baadaye kwamba Besigye
aliachiliwa na kupelekwa nyumbani kwake, akisema walimzuia kiongozi huyo
wa upinzani kuingia eneo la usalama ambalo raia hawakuruhusiwa.
Ingawa Besigye aliachiwa huru, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje
wa Marekani John Kirby alisema kuachiwa kwake hakufuti ukweli kwamba
alikatwa.
![]() |
| John Kirby, Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani |
Kirby aliongeza kusema kwamba Marekani pia ina wasiwasi kuhusu
kufunguliwa kuchelewa vituo vingi vya kupigia kura, pamoja na hatua ya
serikali ya Uganda kuifungia mitandao kadhaa mashuhuri ya kijamii na
mitandao ya kutuma fedha kupitia simu za mkononi siku ya uchaguzi hapo
jana. "Tunaendelea kuihimiza serikali ya Uganda pamoja na vyama vyote
vya siasa na wafuasi wao kujiepusha na vitendo zaidi au kauli zinazoweza
kusababisha machafuko zaidi au watu kufa."
Ukiukaji wa haki za binaadamu
Wakati haya yakiarifiwa, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na
masuala ya haki za binaadamu nchini Uganda, Uchenna Emelonye, alisema
kufungiwa mitandao ya kijamii wakati wa upigaji kura kuna athari zake
katika haki za binaadamu.
"Bila shaka suala la kutia wasiwasi katika ofisi yetu ni ukweli kwamba
serikali ya Uganda imeifungia mitandao ya kijamii, ukiwemo mtandao wa
WhatsApp. Hii ina athari katika haki za binaadamu na tumelijadili suala
hili na maafisa wanaohusika.
![]() |
| Foleni ya wapigaji kura kituo cha Nasuti, wilaya ya Mukono |
Fujo za hapa na pale
Raia wa Uganda walisimama katika foleni ndefu katika vituo vya kupigia
kura, huku upigaji kura ukianza kuchelewa kwa sababu vifaa vya kupigia
kura vilichelewa kufikishwa vituoni.
"Wengi wetu tumejitokeza kupigia kura mageuzi, lakini serikali hii ina
mipango ya kubakia madarakani," alisema Robert Ssebaggala, mpigaji kura
wa mjini Kampala. "Lakini sharti nipige kura kupigania haki zangu,
Museveni lazima aondoke madarakani," akaongeza kusema mwanamume huyo
mwenye umri wa miaka 53.
Muda wa kupiga kura uliongezwa katika wilaya mbili baada ya vituo
kufungwa. Amama Mbabazi, ambaye pia anawania urais, alisema
kucheleweshwa kwa upigaji kura huenda ni njama ya makusudi kwa kuwa
hakuna sababu za msingi kufanya hivyo.
Matukio ya machafuko ya hapa na pale yameripotiwa. Msemaji wa polisi
Patrick Onyango alisema polisi walitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya
wapigaji kura kadhaa katika kitongoji kimoja cha mjini Kampala, na
kuwakamata wawili kwa sababu walijaribu kuwazuia wengine kupiga kura na
kuzua vurugu.
Mwandishi:Josephat Charo/dpae/afpe
Mhariri:Grace Patricia Kabogo



Post a Comment Blogger Facebook